Kwa mujibu wa Idara ya tarjuma ya Shirika la Habari la Hawza, Muungano wa “Mustaqillun” wa Iraq umetoa taarifa kuhusu kusitishwa safari za ndege za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuelekea Iraq.
Muungano huo umetangaza katika taarifa yake kuwa: Tunalaani na kukemea vikali kusitishwa safari za ndege za mashirika ya ndege ya Iran kuelekea viwanja vya ndege vya Iraq, na hatukubali suala hili lishughulikiwe kwa namna inayotoa taswira kwamba uamuzi wa Iraq uko chini ya amri kutoka nje, au kwamba maslahi ya wananchi na uhusiano wa Iraq na majirani zake unaweza kusimamishwa kutokana na shinikizo la nje.
Muungano huo umeeleza: Ukuu wa mamlaka ya Iraq si kauli inayokumbukwa katika hotuba na kisha kuachwa wakati wa kuifanyia maamuzi. Haikubaliki kuchukuliwa hatua yenye madhara kama haya bila kuzingatia matakwa ya wananchi wa Iraq, au bila kuwajali wale ambao safari zao zimevurugwa na maslahi yao kuathirika, madhara ya kusitishwa safari hizi yamewafikia pia wasafiri na waumini wa Iraq na Iran, na yamefanya ufikiwaji wa Ataba na maeneo matakatifu ya ziara katika nchi hizo mbili kuwa mgumu, huku yakiwaongezea mzigo wagonjwa, wanafunzi na familia; kana kwamba mahusiano haya ya kidini na kibinadamu yanaweza kuwa gharama ya migogoro ambayo wananchi hawana uhusiano nayo.
Muungano huo umeongeza: Wakati Muungano wa Mustaqillun ukisisitiza kwamba ujirani mwema na kulinda maslahi ya pande zote ni miongoni mwa misingi thabiti ya maslahi ya kitaifa, unaiomba Serikali ya Iraq ipitie upya hatua hii mara moja na iruhusu safari za ndege za mashirika ya ndege ya Iran kuelekea viwanja vya ndege vya Iraq kuanza tena.
Muungano huo umesisitiza: Hatutakubali wananchi wa Iraq walipie gharama ya uamuzi ulio nje ya matakwa yao, au kupunguzwa mamlaka ya nchi yao juu ya ardhi yake na viwanja vyake vya ndege.
Maoni yako